Wateja ni msingi wa biashara, umeshawahi kujiuliza je biashara inaweza kwenda bila wateja? Bila wateja wa kuwauzia bidhaa au kutoa huduma biashara haiwezi kuwepo. Wajasiriamali wanahangaika na biashara zao kwakuwa wanaamini watapata wateja.
Wateja ni kila kitu katika biashara. Hospitali, vyuo, hoteli, daladala, magazeti, radio na biashara mbalimbali unazozifahamu zote zinahitaji wateja ili ziweze kuendelea. Ukosefu wa uelewa kuhusu wateja ni moja ya sababu zinazofanya biashara zianguke na kufungwa baada ya kuanzishwa.
Pamoja na changamoto katika soko bado wajasiriamali wanashindwa kuelewa ni kwa namna gani wanaweza kukidhi mahitaji ya wateja wao.
. Fanya utafiti wa mahali pazuri pa kufanyia biashara.
Eneo ambalo biashara ipo ni jambo la msingi sana katika kuwavutia wateja na kujenga ufanisi katika biashara. Ni vyema pia kutambua si kila biashara inafaa kwa kila eneo na vilevile si kila eneo linafaa kwa kila biashara!
Unaweza kulalamika kwamba biashara sio nzuri na mambo hayaendi lakini kumbe mwanzo wa yote ni biashara yenyewe kutokuwa kwenye eneo sahihi, haya ni makosa yanayofanywa na wajasiriamali wengi hivyo chagua eneo sahihi kwaajili biashara yako.
Inawezekana upatikanaji wa maeneo ya biashara hasa maeneo mazuri yanahusisha gharama kubwa katika upatikanaji wake, ni muhimu ufanye tathmini ya uhusiano wa eneo na aina ya biashara unayotegemea kufanya.
. Tambua wateja halisi wa biashara yako.
Je ni wapita njia? Unapoamua kufanya biashara fikiria pia juu ya walengwa halisi wa biashara husika, ingawa wanaweza kutokea wateja mbalimbali lakini lazima walengwa wawepo.
Elewa wateja ni msingi wa mafanikio katika biashara yako, jiulize wateja wako ni akina nani, nini kitawasukuma kuja kununua kwako, je ni watu wenye uwezo wa kifedha kwa kiasi gani na wanatoka wapi? Ukijiuliza maswali haya utaweza kufahamu namna ya kubuni biashara nzuri kwaajili ya wateja wako.
Kwa mfano ukienda benki kuna akaunti za aina mbalimbali kutokana na madaraja ya wateja, kuna akaunti za makampuni, akaunti za watoto n.k. Hivi ndivyo na wewe kama mjasiriamali unatakiwa kufikiria kuhusu aina ya wateja wako.
Ni muhimu kuwa na mchanganuo wa aina mbalimbali za wateja unaowalenga katika bishara yako. Haiwezekani ‘’nguo’’ moja ikamtosha kila mtu! Kwa mfano kama umeamua kufungua duka la nguo jiulize walengwa ni kina nani na utawapataje?
Kumbuka soko ni kubwa sana na wateja ni wengi, hivyo wewe kama mjasiriamali unatakiwa kuwaainisha wateja wako katika matabaka kutokana na aidha mila, desturi, uwezo wa kiuchumi, jinsia, elimu, au maeneo wanayotoka.
. Ainisha bei stahiki ya bidhaa zako.
Ni muhimu kwa mjasiriamali kupanga bei za bidhaa zake kwa namna ambayo itawaridhisha wateja. Pamoja na kuwa na soko la bidhaa zako, yakupasa kuwa na bei zenye kukubalika miongoni mwa wateja wako.
Vilevile angalia uwezo wa kiuchumi wa eneo husika, zipo baadhi ya bidhaa ambazo bei zake zinaeleweka na zipo bidhaa ambazo bei zake hutofautiana kutokana na mahali. Hii yote inatokana na uwiano wa kiuchumi, mila, desturi na tamaduni za jamii husika.
Ni muhimu kuelewa na kukumbuka kuwa wewe kama mjasiriamali una wajibu wa kuwatafuta wateja, kuhakikisha wanakuja kwako na si wateja wakutafute wewe. Wapo wajasiriamali baada ya kuanzisha biashara wanakaa kusubiri waje badala ya kuwatafuta
. Wafahamu washindani wako.
Tafuta namna ya kuwafahamu washindani wako kujua wanafanya nini kukidhi mahitaji ya wateja wao, ni muhimu kujifunza mabaya na mazuri ya washindani wako bila kuwachukulia washindani wako kama maadui.
Ni busara mara kwa mara ujiulize ni mahali gani kwingine wateja wako wanapoweza kununua bidhaa kama zako unazouza? Ni muhimu kufanya hivyo kwasababu wateja wengi hupenda kwenda mahali penye unafuu kupata bidhaa wanazohitaji na wapo tayari kwenda popote.
Pamoja na kuwafahamu washindani wako yakupasa kama mjasiriamali kuwa tofauti na washindani wako. Kuwa mbunifu kwa kutafuta namna ambayo itaweza kukutofautisha na washindani wako hata kama wote mnauza bidhaa zinazofanana.
Kuna namna mbalimbali ambazo unaweza kujitofautisha na washindani kama vile utoaji wa punguzo la bei kwa wateja wanaonunua bidhaa kwa kiasi kikubwa, utayari wa kupeleka bidhaa hadi eneo husika la mteja na njia nyinginezo.
. Biashara ni matangazo, jinadi kwa watu.
Je biashara yako inafahamikaje kwa watu? Tafuta namna mbalimbali zenye gharama nafuu ili kuweza kufikisha ujumbe wa kile unachokifanya. Mfano jaribu kuweka matangazo madogo madogo ya biashara yako kwenye magazeti, majarida na mabango makubwa ya biashara mbalimbali. Mbinu hii ya kutangaza biashara imewasaidia wengi kupata wateja wengi katika biashara zao.
. Fanya tathmini ya biashara yako.
Ni vizuri kujiuliza maswali kama vile, je una wastani wa wateja wangapi kwa siku, juma au mwezi? Je unafikiri kuna mwelekeo wa kupata wateja zaidi wa kununua bidhaa zako siku zijazo?
Je wateja wako wapo tayari kununua bidhaa zako kwa bei uliyopanga? Je ni kwa kiasi gani wateja wako wanaridhishwa na huduma unazotoa? Je mahitaji ya bidhaa unazouza yakoje, je ni ya msingi, lazima au ni ya kujifurahisha. Je unaridhia kwa kiasi gani kiwango cha mauzo au mapato yako?
Kama ambavyo tumeweza kuona wateja ni msingi wa biashara yako, wewe kama mjasiriamali jitahidi kufanya lolote linalowezekana uweze kubaki na wateja ulionao, unapofikiria biashara yako fikiria utoaji wa huduma bora, uendeshaji makini wa biashara ili isife kwa kuepuka kupata hasara zinazoepukika, kukuza mtaji na kupanua biashara yako
No comments:
Post a Comment